
Mchekeshaji maarufu DJ Shiti ameibua kicheko mitandaoni baada ya kujitokeza kwa njia ya ucheshi kumuombea VJ Patelo, kufuatia tetesi kwamba ndoa yake na mkewe Dee imeingiwa na ukungu.
Kupitia video ambayo kwa sasa inasambaa, DJ Shiti amesikika akitumia lugha tata ya Sheng kuomba mikosi imuondokee Patelo. Lugha hiyo, iliyojaa maneno ya ucheshi na misemo isiyoeleweka kirahisi, imewafanya mashabiki wengi kucheka huku wengine wakisema maombi hayo ndiyo dawa ya jini mkata kamba linalodaiwa kuingia kwenye ndoa ya Patelo.
“Baba nakabidhi Patelo mikono mwako, chude ngenje, chude ngenje siku zombotote ngezo zikuje nyingi. Ngezo zikuje kama zombotote apate shagla kama zombotote. Nakataa maroho ya chang’ili nakataa roho ya black devil. Nambariki na roho ya Captain Morgan siku zombotote. Gota hatujawahi bugunda!!”, Alisikika akisema kwenye video inayosambaa mtandaoni.
Video ya DJ Shiti imekuja siku chache baada ya ile iliyosambaa ikimuonyesha Dee akimzaba kofi Patelo walipokuwa katika nightclub moja jijini Nairobi, tukio lililoibua tetesi kwamba ndoa yao inakumbwa na changamoto.
Hata hivyo, VJ Patelo mwenyewe amekanusha vikali madai hayo, akisisitiza kuwa ndoa yake iko imara na haina misukosuko. Akiwa amekasirishwa na tetesi hizo, Patelo aliwaambia wakosoaji wake wajishughulishe na maisha yao badala ya kufuatilia mambo ya kifamilia yake.
Kauli ya Patelo imeonekana kama onyo kali kwa wanaoendeleza uvumi mitandaoni, huku DJ Shiti akigeuza sakata hilo kuwa kichekesho kwa maombi yake ya Sheng ambayo yamewachekesha wengi.