Jaribio la kupatanisha wanandoa waliokosana kupitia kipindi kipya cha mtangazaji na mchekeshaji maarufu Oga Obinna limegonga mwamba baada ya mwanamke mmoja kukataa msamaha wa mumewe hata baada ya kufikishiwa maua na ujumbe wa msamaha
Katika tukio hilo, Obinna aliwasili akiwa amebeba maua akiandamana na mpiga tarumbeta kwa lengo la kumfikishia mwanamke huyo zawadi kutoka kwa mumewe kama ishara ya msamaha. Hata hivyo, badala ya furaha na maridhiano, alijipata akikabiliwa na hasira na lawama.
Mwanamke huyo alikataa zawadi na msamaha huo, akimtuhumu mume wake kwa kumtelekeza kwa muda mrefu na kutochukua simu zake. Aidha, alimshtumu Obinna kwa kuhujumu ndoa yake kupitia kushiriki katika mpango huo wa kuwapatanisha wapenzi waliokosana.
Obinna, akibaki mdomo wazi, alilazimika kujitetea akisema hakuwa anajua undani wa mgogoro huo. Alifafanua kwamba jukumu lake lilikuwa tu kuwasilisha zawadi kupitia kipindi chake kipya, ambacho kimebuniwa kuwaleta pamoja wapenzi waliokosana..