Msanii wa muziki kutoka Kenya Dufla Diligon ameonyesha furaha na shukrani zake baada ya kurejea tena kwenye ramani ya muziki kupitia ngoma za “Donjo Maber” na “Rumours”, ambazo zimepata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki, licha ya kipindi kirefu cha kutokuwa kwenye mwanga wa umaarufu.
Kupitia mitandao yake ya kijamii, Dufla amesema nyimbo hizo zimempa nguvu mpya na kumrudisha kwenye mzunguko wa wasanii wanaozungumziwa, akibainisha kuwa kurejea kwake si bahati bali ni matokeo ya subira, juhudi na kuamini kipaji chake.
Dufla amemshukuru Mungu kwa mafanikio hayo, akisema safari yake ni ushahidi kwamba hata yaliyoonekana kuwa magumu yanaweza kubadilika na kuwa mafanikio makubwa.
Lakini pia amemshukuru msanii Iyanii, akimtaja kama msanii mwenye kipaji kikubwa zaidi, huku akiwashukuru maprodyuza pamoja na mashabiki waliompa sapoti kwa kipindi chote cha mwaka.
Hata hivyo amewahakikishia mashabiki wake kuwa bado ana mambo makubwa mwaka mpya wa 2026, akiahidi nyimbo kali na miradi mikubwa zaidi itakayothibitisha kuwa bado ana nafasi muhimu kwenye tasnia ya muziki nchini Kenya.