
Mwanamuziki nyota wa Uganda, Eddy Kenzo, ameeleza masikitiko makubwa dhidi ya waandaaji wa Coffee Marathon kwa kumpa kipaumbele msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz, badala ya kuwatambua na kuwaunga mkono wasanii wa ndani ya nchi.
Katika mahojiano aliyofanya na kituo cha televisheni cha ndani mapema wiki hii, Kenzo alieleza kusikitishwa kwake na taarifa kuwa Diamond alilipwa shilingi milioni 750 za Uganda kwa kushiriki katika tamasha hilo, kiasi anachokiona kuwa ni kikubwa mno, hasa ikizingatiwa kuwa wasanii wa Uganda wamekuwa wakipuuzwa kwenye matukio ya kitaifa.
Katika hatua nyingine, alikosoa maisha ya kifahari aliyotengewa msanii huyo kutoka Tanzania huku wasanii wa Uganda wakiachwa bila msaada au kutambuliwa. Kenzo amesisitiza kuwa hawezi kuiga chochote kutoka kwa Diamond Platnumz licha ya shinikizo zinazotolewa na Waganda kuwa wasanii wao wanapaswa kuboresha chapa zao na muonekano wao wa kisanii ili kuendana na nyakati zilizopo.
“Mimi siwezi kuiga chochote kutoka kwa Diamond Platnumz. Hayo mambo wanayosema kuhusu chapa na kila kitu, siwezi kuwa hivyo. Siwezi kuanza kuvaa minyororo ya dhahabu ishirini, malezi yangu hayakuniandaa kwa hilo. Siwezi kuishi maisha ya kifahari wakati watoto wa Ghetto wanateseka. Bora nitumie pesa hizo kuboresha maisha yao,” alisema Kenzo katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini Uganda.
Diamond Platnumz na Eddy Kenzo wanachukuliwa kuwa miongoni mwa wasanii wakubwa zaidi wa Afrika Mashariki kimataifa. Hata hivyo, Kenzo anaonekana kuwa mbele katika upande wa tuzo za kimataifa alizoshinda, ikiwemo uteuzi wake wa kihistoria katika Tuzo za Grammy.