Mchekeshaji na mwanaharakati wa kijamii Eric Omondi amesema kuwa kuzaliwa kwa Kenya mpya ni jambo lisiloweza kuzuilika, akieleza kuwa kizazi kipya kinachojitokeza sasa ni cha Wakenya wasioangalia ukabila, bali umoja na mabadiliko.
Kupitia ujumbe wake Instagram, Omondi amesema kuwa “The birth of a new Kenya is inevitable”, akisisitiza kuwa taifa la Kenya linaingia katika kipindi kipya cha mageuzi ya kijamii na kisiasa ambacho kitavunja ukabila, ufisadi, na tamaa ya mali.
Eric anaamini kuwa kizazi kipya cha Wakenya kimeamka na kiko tayari kupigania taifa lenye haki, usawa na uwajibikaji. Kwa mujibu wake, mabadiliko haya hayatategemea wanasiasa wa jadi, bali vijana na raia wa kawaida wanaotaka kuona Kenya yenye amani na maendeleo.
Kauli hiyo imekuja muda mfupi baada ya Omondi kuzindua kampeni maalum ya kuhamasisha vijana katika vyuo vikuu kujisajili kama wapiga kura kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Kampeni hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa vijana katika maamuzi ya kisiasa na kuhakikisha sauti yao inasikika kwenye mustakabali wa taifa.