Familia ya aliyekuwa mwimbaji wa injili Betty Bayo imevunja ukimya na kufunguka kuhusu chanzo cha kifo chake kilichotikisa mashabiki na wadau wa muziki wa injili nchini Kenya.
Kupitia taarifa rasmi kwa vyombo vya habari, familia imethibitisha kuwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa damu aina ya leukemia, ambao alikuwa akipambana nao kwa muda kabla ya hali yake kuzorota wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa familia, Betty Bayo alilazwa katika High Dependency Unit (HDU) ya Hospitali ya Kenyatta baada ya kuanza kuugua ghafla, lakini juhudi za madaktari kumwokoa hazikufaulu.
Familia imeongeza kuwa marehemu alipigana kwa ujasiri na ugonjwa huo hadi dakika za mwisho, huku wakiomba umma kuheshimu faragha yao wakati huu wa majonzi.
Hata hivyo wamesema mipango ya mazishi inaendelea, na mwili wa marehemu umehamishwa kutoka Hospitali ya Kenyatta hadi KU Referral Funeral Home.