Entertainment

Halima Namakula Awaasa Wasanii wa Kike: “Msikimbilie Kujifungua, Jengeni Kwanza Ndoto Zenu”

Halima Namakula Awaasa Wasanii wa Kike: “Msikimbilie Kujifungua, Jengeni Kwanza Ndoto Zenu”

Mwanamuziki mkongwe na anayeheshimika sana katika tasnia ya burudani nchini Uganda, Halima Namakula, ameendelea kudhihirisha hekima yake kwa kutoa ushauri mzito kwa wasanii wa kike wa kizazi kipya.

Katika mahojiano ya hivi karibuni, Namakula aliwahimiza wasanii wa kike kutokukimbilia suala la kuanzisha familia mapema, badala yake wajikite kwenye masuala yakukuza taaluma zao za muziki na kufurahia maisha yao wakiwa wangali wachanga.

“Hamstahili kuharakisha kujifungua. Jengeni kwanza kazi zenu, mfurahie maisha yenu. Uzazi una wakati wake, na utakapofika, mtakuwa mmejiandaa vya kutosha,” alisema Namakula kwa msisitizo.

Katika ushauri wake, Namakula alimtaja msanii maarufu Spice Diana, ambaye amekuwa akikumbwa na shinikizo la mashabiki wanaomtaka kuwa mama, akisema hapaswi kuogopa shinikizo hizo, kwani bado ana muda mrefu wa kuwa mama. Alipendekeza Diana afikirie kuwa na familia baada ya kufikisha miaka thelathini.

“Diana ana muda mwingi. Aendelee na kazi yake, apate mafanikio zaidi, na afikirie kuwa mama akifikisha miaka thelathini.”

Namakula alieleza kuwa msingi thabiti wa kazi ya muziki unaweza kuwa nguzo imara kwa maisha bora ya watoto siku za mbeleni. Alisisitiza kuwa mafanikio ya sasa yatawasaidia wasanii hao kuwapa watoto wao maisha yenye usalama, uthabiti na fursa.

Kwa mujibu wake, uzazi ni baraka, lakini unahitaji maandalizi ya kiakili, kifedha, na kimazingira. Hivyo basi, kujijenga kwanza ni njia bora ya kuwajibika kama mzazi katika siku za usoni.

Kwa miaka mingi, Halima Namakula amekuwa mlezi, mshauri, na mfano kwa wasanii wengi wa kike katika ukanda wa Afrika Mashariki. Anaamini kuwa mafanikio hayaji kwa bahati, bali kwa mipango thabiti, nidhamu, na subira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *