Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Harmonize, amefunguka wazi kuhusu hisia zake binafsi na kile alichokuwa akikikosa zaidi kwa Kajala Masanja kipindi walipokuwa wametengana.
Akizungumza kwa uwazi, Harmonize amesema kuwa licha ya Kajala kujulikana kwa urembo wake unaovutia wengi, kitu kikubwa zaidi alichokuwa akikimiss ni utu na tabia yake, akisisitiza kuwa utu wa Kajala ulimvutia na kumgusa kuliko sura au muonekano wa nje.
Kwa mujibu wa Harmonize, Kajala ni mwanamke mwenye moyo wa kipekee, anayejali na anayejua namna ya kuishi na watu, sifa ambazo zilimfanya ahisi pengo kubwa walipotengana. Ameongeza kuwa uamuzi wa kurudiana haukutokana na mvuto wa macho bali ni thamani ya utu, mawasiliano na namna wanavyoelewana.
Ikumbukwe kuwa mwaka 2022, Harmonize aliwahi kumvisha Kajala pete ya uchumba katika sherehe ndogo ya kifahari iliyofanyika kwenye moja ya hoteli kubwa nchini Tanzania. Hata hivyo, mahusiano yao yalivunjika baadaye kufuatia mgogoro mzito uliosababisha kila mmoja kumtupia mwenzake maneno na shutuma nzito hadharani.