Msanii nyota wa Bongo Fleva, Harmonize, ametambuliwa rasmi na Recording Academy kwa kazi nne alizoshiriki ambazo zimezingatiwa katika mchakato wa Tuzo za Grammy za mwaka 2025.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmonize ameonyesha furaha yake kwa hatua hiyo, akisema kuwa mwaka 2025 umeanza vyema na akawahimiza mashabiki wake waendelee kusukuma gurudumu la mafanikio zaidi.
Kazi zake nne zilizotajwa kuzingatiwa katika mchakato wa Tuzo za Grammy za 68 kwenye kipengele cha Best African Music Performance ni pamoja na Furaha, Finally aliyomshirikisha Miri Ben, Simuoni aliyomshirikisha AY, na Me Too aliyomshirikisha Abby Chams.
Hii ni mara ya kwanza kwa Harmonize kuwa na nyimbo kadhaa kufikishwa katika hatua ya kuchukuliwa kwa maamuzi ya awali na Recording Academy, jambo linaloonyesha jinsi muziki wa Bongo Fleva unavyopata nafasi kubwa zaidi kwenye jukwaa la kimataifa.