Entertainment

Harmonize Ajibu Kwa Hasira Tuhuma za Kumdai Ibraah

Harmonize Ajibu Kwa Hasira Tuhuma za Kumdai Ibraah

Staa wa muziki wa Bongo Fleva na mwanzilishi wa lebo ya Konde Gang, Rajab Abdul Kahali maarufu kama Harmonize, hatimaye ameweka wazi uhusiano wa sasa kati yake na aliyekuwa msanii wake, Ibraah. Hili ni baada ya tetesi nyingi kuzagaa kuhusu kuvunjika kwa ushirikiano wao uliodumu kwa miaka minne.

Kupitia mitandao yake ya kijamii, Harmonize alithibitisha rasmi kuwa Ibraah si sehemu ya Konde Gang tena, na sasa anafanya kazi kama msanii huru. Katika kueleza hali halisi ya kuondoka kwa Ibraah, Harmonize alikanusha vikali madai kwamba alimtoza msanii huyo kiasi cha Shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya kuvunja mkataba wao.

“Ni kweli mdogo wangu Chinga alinipigia simu na kuniambia anataka kutoka Konde Gang. Nilimtakia kila la kheri, lakini nikamshauri azungumze na viongozi wa lebo iwapo anahitaji kununua catalogue ya nyimbo zake,” alisema Harmonize huku akisisitiza kuwa hakuna madai yoyote ya kifedha baina yao.

Harmonize aliongeza kuwa madai yaliyosambaa mitandaoni kuhusu deni hilo hayana ukweli wowote na yamekuwa yakimchafua bila sababu.

“Simdai Ibraah pesa hiyo, na siwezi kupenda pesa yangu ije kunichafua mimi mwenyewe,” alisema kwa msisitizo.

Katika upande mwingine wa mazungumzo hayo, Harmonize alifunguka kuhusu mustakabali wa Konde Gang, akieleza kuwa lebo hiyo iko tayari kufungua milango kwa vipaji vipya. Alisema kuwa licha ya changamoto, Konde Gang bado inaendelea na jukumu lake la kuibua na kulea wasanii chipukizi wenye ndoto kubwa.

Taarifa hiyo imeibua hisia mbalimbali kutoka kwa mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva, wengi wakimpongeza Harmonize kwa ukomavu wake wa kiuongozi na namna alivyosimamia suala hilo kwa hekima na utulivu.

Kwa sasa, wadau wa muziki na mashabiki kwa ujumla wanasubiri kuona Ibraah atajielekeza wapi akiwa kama msanii huru, huku nafasi mpya zilizofunguliwa ndani ya Konde Gang zikisubiri kujazwa na vipaji vipya vinavyokuja na njaa ya mafanikio.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *