Staa wa muziki wa Bongo Fleva Harmonize ameamua kumpa Mbosso maua yake akiwa angali hai, kufuatia gumzo lililoibuka mitandaoni ambapo mashabiki walidai Mbosso alimfunika kwenye wimbo wao mpya uitwao Leo.
Kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram, amesema maoni ya mashabiki hayamshangazi, kwani anamfahamu Mbosso kama msanii mwenye mtunzi anayeweza kuwasilisha ujumbe kwa undani mkubwa. Ameongeza kuwa kipaji hicho ndicho kinachoufanya wimbo Leo kusikika tofauti na kuvutia mashabiki wengi.
Aidha, Harmonize ameonesha heshima kubwa kwa ubunifu wa Mbosso, hasa katika matumizi ya misemo ya ndani na maneno yenye ladha ya asili, akisema baadhi ya misemo iliyotumika kwenye wimbo wao ni adhimu na haiwezi kupatikana kirahisi hata kwa utafutaji wa mtandaoni. Kwa mujibu wake, hilo linaonesha ukubwa wa kipaji na uzoefu wa Mbosso katika sanaa ya muziki.
Kwa kumalizia, Harmonize amesema kuwa uzoefu wake wa kuimba umefikia hatua ambayo kila anaposhirikiana na msanii wa nyumbani, sauti zao huonekana kama zimechanganywa na msanii kutoka mataifa ya nje, hususan Marekani. Ameeleza kuwa hali hiyo sio mara ya kwanza kutokea, akitolea mfano kolabo zake na wasanii kama Rayvanny na Marioo.