Msanii nyota wa Bongofleva, Harmonize, ametangaza rasmi kuwa ataachia albamu yake mpya mwezi Januari 2026, licha ya awali kuiahirisha kutokana na hali ya mashabiki kuwakataa baadhi ya wasanii waliojihusisha na siasa zilizosababisha machafuko nchini Tanzania.
Kupitia taarifa yake, Harmonize amesema sasa kila kitu kipo tayari na amewataka mashabiki wake kukaa mkao wa kula ili kuipokea albamu hiyo mpya aliyoipa jina “31”, akiahidi itakuwa kazi kubwa yenye ubora wa hali ya juu na ladha tofauti ya muziki.
Sanjari na hilo, msanii huyo pia ametangaza kufanya ziara kubwa ya kimataifa kuanzia Machi 15, itakayomkutanisha na mashabiki wake katika mataifa ya Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Sudan Kusini, Rwanda pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kauli ya Harmonize imekuja baada ya kutangaza kuwa anatarajia kuwapa mashabiki wake zawadi ya nyimbo sita maalum kabla ya sikukuu za Krismasi za mwaka huu, hatua ambayo imeongeza hamasa na matarajio makubwa kuelekea albamu hiyo mpya.