
Mfanyabiashara anayejiita Madollar Mapesa, amezua gumzo baada ya kuweka wazi kwamba anamdai mrembo na mfanyabiashara, Huddah Monroe, shilingi milioni 6 za Kenya.
Kupitia Instagram yake, mkopo huo ulitolewa kupitia meneja wake na ulitarajiwa kurejeshwa kwa wakati, lakini hadi sasa haujalipwa. Mapesa amesema kwamba mara nyingi huwa anawasaidia watu wengi kupata mikopo mikubwa kwa masharti nafuu kuliko benki au taasisi nyingine za kifedha, akisisitiza kuwa amewaokoa wengi dhidi ya kupoteza mali na biashara zao kwa sababu ya minada.
Hata hivyo, amesema licha ya ukarimu huo, baadhi ya watu maarufu wamekuwa wakikosa kuheshimu makubaliano ya kurejesha mikopo kwa wakati. Madollar ameonya kuwa ana ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai yake endapo Huddah atakanusha.
Pia ametuma ujumbe kwa wadaiwa wengine anaowadai akiwataka kulipa kabla hajaanza kampeni za kuwataja majina hadharani.
Taarifa hizi zimechochea mjadala mkubwa mitandaoni, ambapo baadhi ya mashabiki wanamtaka Huddah kujitokeza na kueleza ukweli, huku wengine wakipuuza madai ya Mapesa wakiyataja kama mbinu ya kutafuta umaarufu.