Telegram imeweka rasmi mfumo mpya wa usalama unaojulikana kama Passkey, hatua inayolenga kuimarisha zaidi usalama wa akaunti za watumiaji wake duniani kote. Mfumo huu sasa unapatikana kwa watumiaji wote wa iOS, Android, macOS na Windows.
Mfumo wa Passkey unamwezesha mtumiaji kuingia kwenye akaunti yake bila kutumia neno la siri (password) au PIN za kawaida. Badala yake, mtumiaji hutumia key maalum inayohifadhiwa moja kwa moja kwenye simu au kompyuta yake. Key hiyo hufanya kazi kwa kushirikiana na teknolojia za biometric kama vile Face ID, Fingerprint (alama ya kidole) au njia nyingine za uthibitisho wa kifaa.
Kwa mujibu wa Telegram, Passkey ni salama zaidi ikilinganishwa na matumizi ya password za kawaida. Hii ni kwa sababu key hiyo haijirudii, haiwezi kutumika kwenye kifaa kingine bila ruhusa, na ni vigumu sana kudukuliwa. Aidha, hata kama mtu atapata password yako ya zamani, hataweza kuingia kwenye akaunti yako bila kutumia biometric zako binafsi.
Hatua hii inalenga kupunguza matukio ya udukuzi wa akaunti, wizi wa taarifa binafsi na udanganyifu wa mtandaoni, ambao umekuwa ukiongezeka siku hadi siku. Kwa mfumo wa Passkey, usalama wa mtumiaji unakuwa umefungamana moja kwa moja na kifaa chake pamoja na utambulisho wake wa kibaiometriki.
Telegram inaungana na makampuni makubwa ya teknolojia kama WhatsApp, Facebook, Google, Apple ID, Spotify na mengineyo ambayo tayari yameanza kutumia au kuimarisha matumizi ya Passkey kama njia mbadala ya nenosiri la kawaida.