LifeStyle

Huddah Monroe Ataka Roboti Badala ya Watu, Alalamikia Uzembe Kazini

Huddah Monroe Ataka Roboti Badala ya Watu, Alalamikia Uzembe Kazini

Mjasiriamali na mwanasosholaiti maarufu wa Kenya, Huddah Monroe, ameibua mjadala mkali mitandaoni baada ya kulalamikia wafanyakazi wake kwa kile alichokitaja kama kukosa akili ya kawaida (common sense) katika kushughulikia mambo madogo kazini.

Katika ujumbe wake uliojaa malalamiko na kejeli kupitia InstaStory, Huddah alieleza kukerwa na kile alichokiita uzembe na ukosefu wa ufanisi, kutoka kwa wafanyakazi wa ngazi ya juu hadi chini. Alisisitiza kuwa hana tatizo na kazi kubwa, bali ni mambo madogo kama usafi na uangalifu wa mazingira ambayo yanamvunja moyo zaidi.

“Nina timu nzima, lakini hakuna anayefikiria kuondoa maua yaliyoanza kuoza mezani. Nitafungua duka la kwanza la roboti Kenya!, Nahitaji clone (nakala yangu) kwa sababu timu yangu haiwezi hata kushughulikia mambo madogo,” aliandika Huddah, akionyesha wazi kutoridhika na utendaji wa kikosi chake cha sasa.

Kauli hiyo imezua hisia mseto kutoka kwa mashabiki na wafuasi wake, baadhi wakimuunga mkono kwa kutaka nidhamu kazini, huku wengine wakimkosoa kwa lugha ya ukali dhidi ya wafanyakazi wake. Wapo pia waliodokeza kuwa kauli yake inaonyesha shinikizo kubwa analokumbana nalo katika kuendesha biashara.

Huddah, anayejulikana kwa ujasiriamali wake na uwazi katika mitandao ya kijamii, amekuwa mstari wa mbele kukuza bidhaa za urembo chini ya chapa ya Huddah Cosmetics, na pia hujulikana kwa mtindo wake wa maisha wa kifahari.

Hadi sasa, hajatoa taarifa nyingine kufuatia malalamiko hayo, lakini ujumbe wake umeonyesha wazi kuwa anataka mabadiliko ya haraka katika timu yake – au roboti wachukue usukani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *