
Jamaa mmoja nchini Kenya ameibua gumzo mitandaoni baada ya kudai kuwa anauza jaketi alilopewa na Rapa Khaligraph Jones, wakati wa onyesho lililofanyika Machakos.
Kwa mujibu wa jamaa huyo, jaketi hilo ni zawadi ya moja kwa moja kutoka kwa Papa Jones. Hata hivyo, amesema sasa amelazimika kuliuza kwa bei ya dola 100 (takribani KSh 13,000) akieleza kuwa ana mahitaji ya kifedha.
Taarifa hiyo imezua maoni tofauti mitandaoni. Baadhi ya mashabiki wameshangazwa na uamuzi wa kuuza zawadi ya msanii mkubwa kama Khaligraph, huku wengine wakisisitiza kuwa mara tu zawadi inapotolewa, mwenye kupokea ana uhuru wa kuamua atalifanyia nini.
Mpaka sasa, Khaligraph Jones hajaweka wazi msimamo wake kuhusu suala hilo, na kuacha mashabiki wakijiuliza kama kweli jaketi hilo ni la ukweli au ni mbinu ya kutafuta kiki.