Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limethibitisha kifo cha mchekeshaji maarufu wa Tanzania MC Pilpili anayefahamika kama Emmanuel Mathias Matebe, kilichotokea Novemba 16, 2025 katika Kituo cha Afya Ilazo jijini Dodoma.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, ACP William Mwanafupa, amesema marehemu alifikishwa kituoni hapo majira ya mchana akiwa katika hali mbaya na alifariki muda mfupi baada ya kuanza kupatiwa matibabu.
Mwanafupa ameeleza kuwa watu watatu waliokuwa kwenye gari ndogo nyeupe walimkabidhi marehemu kwa msaidizi wake, bila kueleza kilichotokea, kisha wakatoweka mara moja. Amesema msaidizi huyo ndiye aliyemkimbiza Marehemu katika kituo cha afya kwa ajili ya huduma za dharura.
Aidha amesema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa MC Pilpili alishambuliwa na watu wasiojulikana, na majeraha aliyopata sehemu mbalimbali za mwili yanasadikiwa kuwa chanzo cha kifo chake.
Hata hivyo amesema uchunguzi unaendelea ili kubaini mazingira ya tukio na kuwatambua wahusika.