
Msanii nyota wa muziki nchini Kenya, Jovial, amefunguka kwa hisia kali kuhusu maisha magumu aliyowahi kupitia kabla ya umaarufu wake, akieleza kuwa aliwahi kuiba kwenye nyumba ya wageni (guest house) aliyokuwa akifanya kazi ili kumudu kulea binti yake mchanga.
Kupitia Insta Story aliyochapisha jana kwenye mtandao wa Instagram, Jovial alisimulia kuwa wakati mmoja aliwahi kufanya kazi kama receptionist kwenye gesti moja huko Saba Saba, Mombasa, na kutokana na hali ngumu ya maisha, alilazimika kuiba mashuka na taulo kutoka gesti hiyo na kuyauza ili kupata pesa za kumtunza mwanawe aliyekuwa na umri wa miezi minne wakati huo.
“Salo ilikuwa kidogo… a mother and child needed to survive. Tukibadilisha sheets na towels, usiku tunaiuza, tunagawanya hiyo doo Gai! Msinihukumu… Mungu hakutaka kuwe na CCTV juu singepata pesa ya maziwa ya mtoto.” aliandika Jovial.
Jovial amesema kuwa, licha ya hayo yote, anakumbuka kwa shukrani hatua aliyopiga maishani na anajivunia kuwa mama ambaye hajawahi kata tamaa. Ameongeza kuwa kumbukumbu hizo humvunja moyo wakati mwingine, lakini pia humkumbusha kuwa bila matatizo hayo, hangejifunza kuwa imara na mwenye msimamo dhabiti kama alivyo leo.
Jovial amewatia moyo mashabiki wake wanaopitia hali ngumu kwa sasa, akiwaambia wakae imara, kwani Mungu hutoa nafasi mpya kwa kila mmoja.
“Cheki mtu akifanikiwa, usione kama hafai kuwa hapo… ni Mungu na yeye tu wanajua place ametoka!” Jovial alihitimisha kwa ujumbe kwa mashabiki na watu wanaopitia changamoto
Kwa sasa Jovial anaendelea kufanya vizuri kwenye muziki, na simulizi yake imewagusa mashabiki wengi ambao wameonyesha heshima kubwa kwa ujasiri wake wa kusema ukweli kuhusu maisha yake ya awali.