Entertainment

Jowy Landa Atoa Majibu Mazito kwa Wakosoaji Wake

Jowy Landa Atoa Majibu Mazito kwa Wakosoaji Wake

Msanii wa muziki kutoka Uganda, Jowy Landa, ameibuka na kujibu ukosoaji anaoupata kutoka kwa baadhi ya mashabiki na wadau wa tasnia ya burudani, akisema kwamba hawamsumbui kwani anaamini wanachukizwa na mafanikio yake.

Kwenye mahojiano na runinga moja nchini Uganda, Jowy alisema kwamba hafuatilii wala kubeba kwa uzito maoni ya wanaomsema vibaya.

 “Mimi hukosolewa kwa sababu mimi ni bora. Watu huwa hawaendi kinyume na wasio na mvuto. Wanaonizungumzia ni kwa sababu wamekasirishwa na ukuaji wangu wa kimuziki,” alisema kwa msisitizo.

Kauli hiyo imezua maoni mseto kutoka kwa mashabiki, hasa ikizingatiwa historia yake ya kutoa kauli kali dhidi ya wasanii wenzake. Mapema mwaka huu, alizua mjadala mkubwa baada ya kumkosoa vikali Spice Diana, akimtuhumu kuwa na kiwango duni cha sauti na kudai kwamba kazi zake hazina ubunifu wa kweli.

Kauli hiyo iliwakasirisha baadhi ya mashabiki wa Spice Diana, lakini upande wa msanii huyo haukujibu hadharani, jambo lililowafanya wengi kusifu utulivu wa timu ya Spice katika kukabiliana na mivutano ya kisanii.

Hata hivyo, Jowy sasa anaonekana kukerwa na ukosoaji wa watu dhidi yake, jambo ambalo limeibua maswali kutoka kwa baadhi ya wachambuzi wa burudani: Je, msanii anayependa kukosoa wenzake hastahili pia kukosolewa?

Wadadisi wa masuala ya muziki wanasema hali kama hizi huibua mjadala kuhusu ukomavu wa wasanii, uwezo wa kujifunza kupitia maoni ya wengine, na uhusiano wa kweli kati ya ubunifu na ukosoaji wa wazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *