
Mwanamitindo maarufu Kim Kardashian ametoa onyo kali kwa aliyekuwa mume wake, msanii Kanye West, akimtaka akae mbali na watoto wao, licha ya kuwa wanashirikiana kwenye ulezi wa pamoja (joint custody). Taarifa hiyo imesababisha gumzo kubwa mitandaoni huku mashabiki wakigawanyika kuhusu hatua hiyo ya Kim.
Kwa mujibu wa vyanzo vya karibu na familia hiyo, Kim ameweka wazi kwamba hataki Kanye awe karibu na watoto wao bila ruhusa maalum, akidai kuwa vitendo na tabia za hivi karibuni za rapa huyo ni zisizotabirika na huenda zikahatarisha utulivu wa watoto.
Hali hiyo inazua maswali kuhusu mustakabali wa mpango wao wa ulezi wa pamoja, hasa ikizingatiwa kuwa Kim na Kanye walikubaliana kushirikiana kulea watoto wao wanne baada ya talaka yao mwaka wa 2022.
Mashabiki mitandaoni wametoa maoni mseto, wengine wakimuunga mkono Kim kwa kutanguliza maslahi ya watoto, huku wengine wakimtetea Kanye na kusema anapaswa kuruhusiwa kuwa sehemu ya maisha ya watoto wake.
Mpaka sasa, Kanye hajatoa kauli rasmi kuhusu tishio hilo, lakini wengi wanatarajia majibu yake, hasa kutokana na historia yake ya kujibu hadharani kupitia mitandao ya kijamii.