Mabingwa watetezi Kenya Police FC wamerejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Soka ya FKF baada ya kutoka sare tasa na AFC Leopards katika dimba la Kasarani.
Katika dakika 90 za mchuano huo, hakuna timu iliyoweza kutikisa nyavu za mwenzake. Hata hivyo, alama moja iliyopatikana imewawezesha Police kufikisha pointi 21, moja mbele ya Gor Mahia, Kakamega Homeboyz, na Posta Rangers ambao wanashikilia nafasi za pili hadi ya nne mtawalia. AFC Leopards kwa upande wao wanabaki katika nafasi ya sita, wakiwa na alama tatu pungufu ya vinara Police.
Katika mechi nyingine, Mara Sugar waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kariobangi Sharks kwenye uwanja wa Awendo Green. Bao la kwanza lilifungwa na Jimmy Owili kipindi cha pili, kabla ya Dennis Cheruiyot kuongeza la pili kupitia mkwaju wa penalti.
Ushindi huo umeinua Mara Sugar hadi nafasi ya tisa kwa alama 17, huku Sharks wakizidi kusalia mkiani baada ya kutoshinda katika mechi zao nane mfululizo.