 
									timu ya taifa ya wanawake ya Kenya, Harambee Starlets, imepata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Gambia katika mechi ya mkondo wa kwanza wa raundi ya mwisho ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika la Wanawake 2026. Mechi hiyo ilichezwa jana kwenye Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo, Nairobi.
Mechi ya mkondo wa pili itafanyika Jumanne ijayo kwenye Stade Lat Dior jijini Thies, Senegal, kwani Gambia haina uwanja unaokidhi viwango vya CAF. Mshindi wa jumla wa mechi hiyo atapata tiketi ya kufuzu WAFCON 2026, itakayofanyika Morocco kuanzia 17 Machi hadi 3 Aprili mwaka ujao.
Rais William Samoei Ruto amewazawadia Starlets shilingi milioni 5 kama motisha ya ushindi huu. Aidha, Rais amewaahidi timu hiyo shilingi milioni 2.5 kwa sare, shilingi milioni 1 kwa kila mchezaji iwapo watashinda kufuzu WAFCON, na shilingi 500,000 kwa kila mchezaji iwapo watafuzu kwa sare.
Huu ni ushindi muhimu kwa Starlets, wakijipanga kuendeleza hadhi ya soka la wanawake nchini Kenya na kuendeleza matumaini ya kufuzu fainali za WAFCON mwaka ujao.”
 
								 
             
             
                             
                             
                             
                             
                             
                             
                            