
Msanii maarufu wa muziki wa hip hop nchini Kenya, Khaligraph Jones, amempongeza DJ Sadic kwa mabadiliko yake ya kimwili baada ya kuongeza uzito kutokana na juhudi zake za mara kwa mara kwenye mazoezi ya viungo.
Katika mahojiano ya hivi karibuni, Khaligraph alielezea jinsi alivyoshtushwa na mabadiliko ya DJ Sadic, ambaye zamani alikuwa mwembamba kupita kiasi.
“Kama DJ Sadic anaweza shona, kila mtu anaweza shona. Alikuwa amekonda anatoshana na uzi,” alisema Khaligraph kwa ucheshi, akimaanisha jinsi DJ huyo alikuwa mwembamba kabla ya kuanza mazoezi.
Mkali huyo wa Ngoma ya Ting Bad Malo” aliendelea kueleza jinsi video za DJ Sadic zikimpa motisha ya kuendelea na mazoezi.
“Huwa naona video zake nasema, huyu jamaa alikuwa amekonda anishinde mimi? Nakimbia zoezi.”
Kauli hiyo imepokelewa kwa vicheko mitandaoni huku mashabiki wakimpongeza DJ Sadic kwa bidii zake na kumpongeza Khaligraph kwa kutambua mafanikio ya wengine.
DJ Sadic, ambaye kwa muda mrefu amejulikana kwa kujituma kwenye tasnia ya muziki, sasa anaonekana pia kuwa mfano bora wa kujali afya ya mwili. Khaligraph, ambaye pia ni mpenzi wa mazoezi, ameendelea kuwa mhamasishaji mkubwa wa maisha ya kiafya miongoni mwa wasanii na mashabiki wake.
Uhusiano huu wa motisha kati ya wasanii hawa wawili unadhihirisha umuhimu wa kujali afya hata katika maisha ya kazi yenye shughuli nyingi.