Mchekeshaji na mtangazaji kutoka nchini Kenya, Oga Obinna, ameibuka mshindi katika kesi ya kashfa ya mtandaoni dhidi ya watangazaji wenzake Massawe Japani, Black Cinderella, na kituo cha redio Radio Jambo.
Kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama uliotolewa jana, Obinna amezawadiwa shilingi milioni sita kama fidia kutokana na maneno ya kumdhalilisha yaliyotolewa kupitia kipindi cha redio mwaka mmoja uliopita.
Kupitia ujumbe wake kwa mashabiki, Obinna ameeleza kuwa sasa amepata fidia ambayo anapanga kuitumia kuanzisha ujenzi wa nyumba yake, akisema ushindi huo unamvutia zaidi kwa sababu umetokana na juhudi za kulinda heshima yake.
Mchekeshaji huyo, amefafanua kuwa madai yaliyotolewa dhidi yake yalikuwa ya uongo na hayakuwa na ushahidi wowote, jambo lililoathiri taswira yake kitaaluma na kibiashara.
Obinna hata hivyo amewataka watumiaji wa mitandao ya kijamii kuwa waangalifu na wanachochapisha mtandaoni, akisisitiza kuwa ni muhimu kuheshimu watu na kuepuka kusambaza taarifa zisizo na msingi kwani hatua za kisheria zinaweza kuchukuliwa.