Entertainment

Malipo ya Diamond Yatikisa Uganda, Wasanii Aibua Mjadala Moto

Malipo ya Diamond Yatikisa Uganda, Wasanii Aibua Mjadala Moto

Msanii mashuhuri wa Uganda, Allan Toniks, amezua gumzo mitandaoni baada ya kulalamikia hadharani kiwango kidogo cha malipo alichopewa kwa kushiriki tamasha moja nchini humo.

Kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Toniks alifunguka kwa hasira kwamba alipewa chini ya dola 1,000, huku akishangaa serikali ya Uganda kutumia shilingi milioni 750 kumlipa staa wa Tanzania, Diamond Platnumz, kwa kushiriki kampeni ya kuhamasisha kahawa.

“Na wanakuja kunipa chini ya dola 1000, nikikataa wanasema najifanya. 750M UGX? Acheni ujinga.” Aliandika kwa hasira.

Kauli ya Toniks ilisambaa kwa kasi, ikizua mjadala mkubwa. Baadhi ya watu walimtetea, wakisema ni wazi kuwa wasanii wa ndani wanadharauliwa na kutopewa thamani stahiki licha ya mchango wao katika kukuza utamaduni wa nchi. Wengine walidai kuwa fedha hizo zingeweza kusaidia miradi ya kijamii au kuimarisha sanaa ya ndani, wakikumbusha kuwa wakazi wa Kiteezi wanahitaji milioni 200 pekee kuboresha maisha yao.

Hata hivyo, wapo waliotetea hatua ya kumleta Diamond, wakisema ni msanii mwenye ushawishi mkubwa barani Afrika na kwamba uwepo wake unaleta mvuto wa kimataifa kwa kampeni ya kahawa. Kwao, hii ni mbinu ya kibiashara na kimkakati ambayo inaweza kusaidia sekta ya kilimo kuvuka mipaka.

Tukio hili limeibua maswali kuhusu vipaumbele vya serikali ya Uganda, thamani ya sanaa ya ndani, na nafasi ya wasanii katika miradi ya kitaifa. Pia limeibua changamoto kwa wasanii wa Uganda kuwekeza zaidi katika kuboresha nembo zao binafsi ili kujiongezea heshima na nafasi kwenye majukwaa ya kitaifa na kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *