
Msanii wa muziki wa hip hop nchini Kenya, Toxic Lyrikali, yuko chini ya shinikizo kutoka kwa mashabiki wake baada ya kuachia nyimbo mbili za mahaba, “Bud Flowers” na “Mpenzi” aliyomshirikisha mwanamuziki Bridget Blue.
Mashabiki wengi wamejitokeza kwenye mitandao ya kijamii wakimtaka arejee kwenye mtindo wake wa zamani wa hardcore gangster rap uliomtambulisha kwenye muziki wa hip hop. Wanaeleza kuwa Toxic Lyrikali alijijengea jina kutokana na mistari mikali yenye simulizi za maisha ya mtaani, hivyo kuingia kwenye muziki wa mapenzi kunahatarisha utambulisho wake wa kisanii.
Baadhi ya mashabiki wameeleza hisia zao kwa kusema kuwa nyimbo za mahaba hazimpendezi msanii huyo, na kwamba anafuata mkumbo wa soko badala ya kudumisha uhalisia wake. Wengine, hata hivyo, wamesema ni kawaida kwa msanii kubadilika na kupanua wigo wa muziki wake ili kufikia hadhira pana zaidi.
Wachambuzi wa tasnia ya muziki wanaona mwelekeo huu unaweza kuwa ni mkakati wa kibiashara, lakini shinikizo la mashabiki linaweza kumlazimisha Toxic Lyrikali kurudi kwenye midundo ya rap kali aliyozoeleka nayo.
Kwa sasa, macho na masikio ya mashabiki yapo kwa Toxic Lyrikali ili kubaini iwapo ataendelea kusimama na mwelekeo wa nyimbo za mahaba, au atasikiliza wito wa mashabiki wake na kurudi kwenye muziki wa mitaani uliomtambulisha.