Mastaa na wadau wa burudani nchini Kenya wamejikuta wakishindwa kufikia mwafaka kuhusu ratiba ya mapokezi na matembezi ya streamer na YouTuber maarufu duniani, IShowSpeed, ambaye yupo kwenye ziara kubwa barani Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa zinazosambaa mtandaoni, wapo wanaodai ziara ya Youtuber huyo ni fursa adhimu ya kuonyesha upande mzuri wa Kenya, ikiwemo utalii, utamaduni, ubunifu wa vijana na maendeleo ya miji, ili kuitangaza nchi kimataifa.
Hata hivyo, kundi lingine linapendekeza IShowSpeed apelekwe pia kwenye mitaa ya mabanda ili kushuhudia uhalisia wa maisha ya baadhi ya wananchi, wakiamini kuwa ziara hiyo inaweza kufungua milango ya misaada au miradi ya kijamii kwa jamii zenye uhitaji. Aidha, wapo content creators wanaotamani kukutana naye ana kwa ana ili kujifunza siri za mafanikio yake kwenye majukwaa ya kidijitali.
Mjadala huo umeibuka zaidi baada ya mastaa wa Afrika Kusini kupokea IShowSpeed kwa ratiba iliyoandaliwa vizuri, na kutumia ujio wake kuitangaza nchi hiyo kimataifa kupitia utalii, utamaduni na maendeleo makubwa ambayo taifa hilo limepiga katika miaka ya hivi karibuni.