
Staa wa muziki wa Bongo Flava, Mbosso Khan, amejitokeza kufafanua madai yaliyoenea mitandaoni kuwa amerejea kijijini kwao Kibiti, mkoani Pwani, kwa sababu maisha yamekuwa magumu baada ya kuondoka katika lebo ya WCB Wasafi.
Kupitia mahojiano na gazeti moja nchini Tanzania, Mbosso amesema kuwa tafsiri iliyotolewa na baadhi ya watu kuhusu picha zake akiwa kijijini ni ya kupotosha na haina ukweli wowote.
“Wakati mwingine huwa nayafurahia sana maisha ya mitandaoni, na wakati mwingine yanakera sana. Mimi kwenda nyumbani kwetu Kibiti ndiyo maisha yangu yamekuwa magumu jamani? Inamaana kila anayeenda kwao basi mjini pamemshinda?” alihoji Mbosso kwa msisitizo.
Msanii huyo ambaye amewahi kutamba na vibao kama “Amepotea”, na “Umechelewa”, aliongeza kuwa safari yake kwenda Kibiti haikuhusiana kabisa na hali ya maisha bali ilikuwa ni kwa ajili ya kutembelea familia, marafiki, na kushughulikia mambo mengine nje ya muziki.
“Nimeenda kule kwa sababu kuna ndugu, jamaa na shughuli nyingine huwa nazifanya kule mbali na muziki. Hii haimaanishi kuwa nimefilisika au maisha yamenibana,” alisema.
Aidha, Mbosso alizungumzia ukimya wake katika tasnia ya muziki tangu aondoke WCB, akieleza kuwa yuko kwenye kipindi cha maandalizi na mipango ya kimuziki kwa umakini zaidi.
“Mashabiki wasiwe na shaka. Kazi zipo tayari na zingine bado zinaendelea kutengenezwa. Nimeamua kujipa muda ili nije kwa kishindo,” alieleza kwa kujiamini.
Kauli ya Mbosso imepokelewa kwa hisia tofauti na mashabiki mitandaoni, huku wengi wakionesha kuungwa mkono kwa uamuzi wake wa kutetea heshima yake na kufafanua ukweli kuhusu maisha yake baada ya kuondoka Wasafi.
Kwa sasa, mashabiki wake wanasubiri kwa hamu kazi mpya kutoka kwake, wakitumaini kuwa atarejea kwenye chati za muziki kwa kishindo kama alivyoahidi.