
Msanii maarufu wa hip hop Meek Mill amezua gumzo mtandaoni baada ya kuchapisha mfululizo wa tweets zenye ujumbe mzito kuhusu shutuma mbalimbali, maisha ya anasa, na heshima ya jina lake.
Katika ujumbe wake, Meek Mill amekanusha vikali madai kwamba aliwahi kushambuliwa au kuibiwa, akieleza kuwa alipokuwa Los Angeles alikutana na watu mashuhuri kama Suge Knight na Big U bila hofu yoyote. Anasema lengo lake lilikuwa kuonyesha vijana kuwa kuna maisha zaidi ya vurugu, hasa kwa jamii ya Weusi.
“Luce Cannon na kile kikao chake na Akademiks kilikuwa mtego mtupu… halafu huyu mtu hana jina, anasema eti alinivamia na kunipora.” Akaongeza: “Nilikuwa nakutana na Suge Knight na Big U nilipokuwa LA… bila kamera wala mbwembwe!” Akisisitiza kuwa madai ya kushambuliwa ni ya uongo.
Meek pia ameeleza kutoridhishwa na mazingira ya sherehe za mastaa, akidai kuwa matumizi ya dawa za kulevya, hasa “coke”, ni jambo la kawaida. Hata hivyo, anasisitiza kuwa yeye hajawahi kulewa hata bangi na anaepuka utegemezi wa vitu hivyo licha ya kuwa na utajiri mkubwa tangu akiwa na miaka 23.
“Kitu cha kushangaza zaidi nilichowahi kuona kwenye sherehe ya Puff ni ‘vibes za coke’… na hii hutokea kwenye hizi sherehe zote.” Akasisitiza msimamo wake kwa kusema: “Nimekuwa na mamilioni tangu nikiwa na miaka 23, sitaki hata kuwa mraibu wa bangi… Sihukumu, lakini naona mambo kwa jicho tofauti!”
Aidha, amekosoa baadhi ya blogu kwa kumhusisha na kesi ya Lil Rod dhidi ya Diddy, akisema kuwa jina lake halikutajwa lakini mitandao imejaribu kumchafua. Anasisitiza kuwa jamii yake haikuamini tuhuma hizo, lakini bado ni shambulio dhidi ya chapa yake.
“Wakati Diddy anakabiliwa na kesi ya FEDERAL, nataka kuibua tena suala la Lil Rod na kesi yake ambayo ilitupiliwa mbali. Hakuwahi kutaja jina langu, lakini blogu ziliendeleza ajenda nzima dhidi yangu.” Akaongeza: “Jamii yangu haikuamini lakini hii ni hujuma dhidi ya chapa yangu… nataka kujua ukweli wa yote haya!”
Kauli hizi kutoka kwa Meek Mill zimezua hisia mseto miongoni mwa mashabiki na watumiaji wa mitandao ya kijamii. Baadhi wamempongeza kwa uwazi wake na msimamo thabiti, huku wengine wakimtaka awe makini na kauli zake, hasa wakati huu ambapo kesi ya Diddy bado iko kwenye mchakato wa kisheria.