
Kampuni ya teknolojia ya Meta Platforms Inc., inayomiliki mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, na Threads, imetangaza kuwa itaunga mkono rasmi juhudi za kuimarisha usalama wa watoto mitandaoni kwa kutekeleza utaratibu wa kuwatambua na kuwadhibiti watumiaji walio chini ya umri wa miaka 16.
Kwa mujibu wa mpango huu mpya, watoto watakaotaka kujiunga na mitandao hiyo watalazimika kuwa na ruhusa ya wazazi au walezi wao kabla ya kufungua akaunti. Hatua hiyo inalenga kulinda faragha na usalama wa watoto, na kuzuia matumizi holela ya majukwaa ya kijamii bila uangalizi wa watu wazima.
Meta imeeleza kuwa itatumia teknolojia ya kisasa, kama vile mifumo ya kiakili ya kutambua umri na nyuso, pamoja na nyaraka rasmi za utambulisho, ili kuhakikisha kuwa taarifa zinazotolewa na watumiaji wachanga ni sahihi. Hii ni sehemu ya jitihada za kudhibiti uongo wa taarifa za umri ambao umekuwa ukitumiwa na watoto wengi kuingia kwenye majukwaa ya kijamii kinyume cha sera za matumizi.
Mpango huu pia unalenga kuhusisha wazazi moja kwa moja katika mchakato wa usajili na matumizi ya mitandao hiyo kwa watoto wao, ili kusaidia kuimarisha usimamizi wa kidijitali majumbani.
Hatua hiyo ya Meta inakuja wakati ambapo mjadala kuhusu usalama wa watoto mtandaoni umeongezeka, na serikali pamoja na mashirika ya haki za watoto duniani kote yamekuwa yakishinikiza mashirika ya teknolojia kuchukua jukumu kubwa zaidi katika kulinda watumiaji wadogo.