Entertainment

Mike Sonko Ajitolea Kufadhili Tamasha la Vybz Kartel Nchini Kenya

Mike Sonko Ajitolea Kufadhili Tamasha la Vybz Kartel Nchini Kenya

Tajiri maarufu na aliyewahi kuwa Gavana wa Nairobi, Mike Sonko, ametangaza kuwa yuko tayari kufadhili tamasha kubwa la msanii nguli wa dancehall kutoka Jamaica, Vybz Kartel, nchini Kenya.

Tangazo hilo limekuja muda mfupi baada ya Vybz Kartel kuonyesha nia ya kutumbuiza barani Afrika, akisema kuwa Kenya ni moja ya nchi anazopendelea kuzuru kwa ajili ya show maalum.

Kupitia ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, Sonko alisema yuko tayari kushirikiana na wadau wa burudani kuhakikisha kuwa tamasha hilo linafanyika, licha ya gharama kubwa inayohusiana na kumleta Kartel. Kwa sasa, ada ya kumuweka jukwaani msanii huyo inakadiriwa kuwa kati ya Shilingi milioni 100 hadi 173 za Kenya.

“Kama Vybz Kartel yuko tayari kuja Kenya, niko tayari kumfadhili. Tufanye hii show iwe ya kihistoria,” aliandika Sonko.

Vybz Kartel, ambaye aliachiliwa kutoka gerezani mapema mwaka huu, ameendelea kudhihirisha ushawishi mkubwa katika tasnia ya muziki wa dancehall duniani. Nyimbo zake maarufu kama Fever, Summertime na Clarks zinaendelea kuvuma mitaani na kwenye redio nyingi humu nchini.

Iwapo tamasha hilo litatimia, litakuwa moja ya maonyesho makubwa zaidi ya kimataifa kufanyika Kenya, na huenda likafungua milango kwa wasanii wengine wa kimataifa kuja kutumbuiza Afrika Mashariki.