
Huenda juhudi za mwanamuziki Dufla Diligon zikagonga mwamba baada ya mrembo Arnelisa Muigai kukataa hadharani ombi la msanii huyo kutaka kuingia naye kwenye mahusiano ya kimapenzi.
Kupitia ukurasa wake wa Instagtam Arnelisa amesikitishwa na kitendo cha Dufla kutumia sarakasi nyingi mtandaoni kwa ajili ya kuteka hisia zake huku akisema kuwa mapenzi hayalazimishwa.
Kauli ya Arnelisa imekuja mara baada ya video kusambaa mtandaoni ikiwaonyesha wasanii KRG The Don na Arrow Boy kwenye moja ya night club wakimliwaza Dufla Diligon ambaye alikuwa analilia penzi la Arnelisa.
Utakumbuka wiki kadhaa zilizopita Dufla alijitokeza wazi na kudai kuwa anatamani kuingia kwenye mahusiano na Arnelisa ambapo alienda mbali zaidi na kuachia wimbo wake uitwao Arnelisa uliokuwa ukisifia urembo wa Arnelisa.
Hayo yamekuja baada ya Arnelisa kutangaza hadharani kukamilisha mchakato mzima wa kuvunja ndoa yake na mwanamuziki bongo fleva Ben Pol.