Mwanamuziki na mtangazaji wa Kenya, Sanaipei Tande, ameeleza kuwa mahusiano ya kweli yanapaswa kujengwa juu ya urafiki na ushirikiano badala ya kuzingatia kile mtu analeta mezani.
Katika mahojiano yake ya hivi karibuni, Sanaipei ameeleza kuwa watu wengi wa kizazi cha sasa (GenZ) wamepoteza maana halisi ya uhusiano kutokana na kuangalia zaidi masuala ya kifedha na faida binafsi. Anasema kuwa uhusiano wa kudumu unahitaji mawasiliano, urafiki, na msaada wa kihisia na kiroho kati ya wawili wanaopendana.
Msanii huyo, anayefahamika kwa nyimbo kama Amina na Najuta, ameongeza kuwa urafiki ndio msingi wa uelewano wa kweli katika mahusiano, kwani hutoa nafasi kwa watu kujifunza na kuelewana kabla ya kuchukua hatua kubwa zaidi.
Kauli ya Sanaipei imepokelewa kwa hisia tofauti mitandaoni, wengi wakimsifu kwa kuzungumzia ukweli kuhusu changamoto za mahusiano ya kisasa.