
Msanii nguli wa muziki kutoka Tanzania, TID (Top In Dar), ameelezea masikitiko yake kuhusu changamoto zinazowakumba wasanii nchini humo, hasa kutolipwa mirabaha yao licha ya kazi zao kuendelea kutumika kwenye vyombo mbalimbali vya habari.
Kupitia mitandao ya kijamii, TID alisema kuwa licha ya wasanii kukosa fursa za mikopo na msaada wa kifedha, hata haki yao ya msingi ya kulipwa mirabaha kwa kazi wanazozalisha haitekelezwi. Alidai kuna zaidi ya shilingi bilioni moja zinazopaswa kuwalipa wasanii lakini hakuna uwazi kuhusu fedha hizo.
Kwa mujibu wa TID, hali hiyo inaonyesha jinsi ambavyo wasanii, licha ya kuwa miongoni mwa watu wanaochangia sanaa, utamaduni, na uchumi wa taifa, bado wanakabiliwa na ukosefu wa heshima na uthamini kutoka kwa taasisi husika.
“Mikopo Tumepigwa Chini Sawa…Basi hata hiyo MiRABAHA haki yetu nayo hatulipwi na Tunajua Kuna Zaidi ya 1 Bilioni sijui hapo tunakosea wapi sisi Wajenga Nchi wenye Vipaji,” Aliandika kupitia Instastory yake.
Kauli yake imezua mjadala mpana kwenye mitandao ya kijamii, huku wapenzi wa muziki na wadau wa sanaa wakimtaka Waziri wa Utamaduni pamoja na taasisi za usimamizi wa mirabaha kutoa majibu kuhusu wapi fedha hizo zimekwama na kwa nini wasanii hawapati stahiki zao.
TID ni miongoni mwa wasanii walioweka historia katika muziki wa Bongo Flava, na amekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya wasanii wenzake kwa muda mrefu