
Mtoto wa rapa maarufu Lil Wayne, anayefahamika kwa jina la kisanii Lil Novi, amezua gumzo mitandaoni baada ya kudai kuwa mafanikio ya rapa Drake yalichangiwa pakubwa na mchango wa baba yake katika uandishi wa nyimbo.
Akizungumza katika mahojiano maalum yaliyopeperushwa hivi majuzi, Lil Novi alisema kuwa Lil Wayne hakuhusika tu kumtambulisha Drake kwa dunia ya muziki, bali pia alihusika moja kwa moja katika kuandika nyimbo zake nyingi zilizomletea umaarufu mkubwa.
“Baba yangu ndiye aliyeweka msingi mzuri kwa Drake. Yeye ndiye aliyemsaidia kuandika nyimbo nyingi za Drake ambazo zimepata mafanikio makubwa,” alisema Lil Novi kwa msisitizo.
Kauli hiyo imeibua mijadala mikali miongoni mwa mashabiki wa hip hop, huku baadhi wakisema kwamba si jambo la kushangaza ikizingatiwa kuwa Lil Wayne ndiye aliyemsaini Drake chini ya lebo yake ya Young Money mwaka 2009, kipindi ambacho Drake alikuwa bado hajajijengea jina kimataifa.
Uhusiano kati ya Lil Wayne na Drake umeendelea kuvutia hisia za wengi, hasa kutokana na ushirikiano wao wa muda mrefu na mafanikio ya pamoja katika muziki. Hata hivyo, madai ya Lil Novi yanaweza kufungua ukurasa mpya wa mjadala kuhusu mchango wa Lil Wayne katika mafanikio ya Drake, ambao kwa sasa ni miongoni mwa wasanii wa hip hop wanaosikilizwa zaidi duniani.
Wakati mashabiki wakingoja kauli ya Drake au Lil Wayne kuhusu suala hilo, ukweli mmoja unabaki palepale, ushawishi wa Lil Wayne katika muziki wa kizazi hiki hauwezi kupuuzwa.