
Mchekeshaji maarufu nchini Kenya, Mulamwah, amenusurika ajali ya barabarani na amethibitisha kuwa yuko salama kupitia ujumbe aliouweka kwenye mitandao ya kijamii.
Katika chapisho hilo, Mulamwah alieleza kwamba tukio hilo lilitokea kwa haraka sana, lakini anamshukuru Mungu kwa kuwa hakuna mtu aliyejeruhiwa.
“Happened so fast. We are grateful to God that no one was injured,” aliandika Mulamwah kupitia InstaStory yake, sambamba na picha ya gari lililoharibika sehemu ya mbele.
Ajali hiyo ilitokea Ijumaa tarehe 20 Juni 2025, wakati mchekeshaji huyo akiwa safarini kwenye shughuli zake za kawaida. Ingawa hakufichua eneo halisi lililotokea ajali hiyo, picha zilizosambazwa mitandaoni zilionyesha gari lake likiwa na uharibifu mdogo upande wa mbele, hali inayodokeza kuwa lilihusika katika mgongano.
Mashabiki wake mitandaoni walijitokeza kwa wingi kumpa pole na kumtakia afueni, huku wengi wakimtaka awe mwangalifu zaidi barabarani. Wengine walitumia fursa hiyo kuwakumbusha madereva kuhusu umuhimu wa tahadhari barabarani, hasa kipindi hiki ambacho mvua zinashuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Mulamwah hakusita kumshukuru Mungu kwa kuendelea kumlinda, akieleza kuwa ingawa tukio hilo lilikuwa la kutisha, anakichukulia kama onyo la kutambua thamani ya maisha na kuwa makini zaidi.
“Ni neema ya Mungu. Tunapaswa kuwa na shukrani kila siku tunayopata nafasi nyingine ya kuamka,” alisema katika mazungumzo mafupi na mashabiki wake.
Tukio hili linakuja wakati ambapo Mulamwah amekuwa akigonga vichwa vya habari kutokana na malumbano ya mitandaoni na aliyekuwa mpenzi wake, Ruth K. Hata hivyo, ajali hiyo imeleta mwelekeo mpya na kumbukumbu ya jinsi maisha yalivyo mafupi na ya thamani.