
Mwanasheria wa mwanamuziki maarufu wa Marekani, Megan Thee Stallion, Alex Spiro, amejitokeza kutoa kauli kali kufuatia taarifa zilizotolewa jana na timu ya mawakili wa Tory Lanez kuhusu kesi ya kumpiga risasi Megan.
Kupitia taarifa kwa jarida la XXL Magazine, Spiro amejibu madai yaliyotolewa katika mkutano wa waandishi wa habari uliandaliwa na mawakili wa Lanez, ambapo walidai kuwa rafiki wa Megan, Kelsey Harris, ndiye aliyempiga risasi msanii huyo – na siyo Tory Lanez kama ilivyodaiwa awali.
Spiro amekanusha vikali madai hayo, akisisitiza kuwa hukumu iliyotolewa dhidi ya Tory Lanez ilifuata mchakato halali wa kisheria.
“Tory Lanez alishtakiwa na kutiwa hatiani na wenzake, na kesi yake ilipitia katika mfumo sahihi wa mahakama. Hili si suala la kisiasa – hii ni kesi ya shambulio la kikatili ambalo lilisikilizwa na kuamuliwa kwa mujibu wa sheria,” alisema Spiro.
Kesi hiyo, ambayo ilivuta hisia za watu wengi kote duniani, ilimalizika kwa Tory Lanez kupatikana na hatia ya kumshambulia Megan kwa kutumia silaha ya moto, tukio lililotokea Julai 2020. Hukumu hiyo ilileta mgawanyiko mkubwa mtandaoni kati ya mashabiki wa pande zote mbili.
Kwa sasa, bado haijabainika kama ushahidi mpya uliodaiwa na timu ya Tory Lanez utawasilishwa rasmi mahakamani kwa ajili ya rufaa au mapitio ya kesi.