
Mwanamuziki Nadia Mukami amedokeza kuja na EP ya pamoja na mchumba wake Arrow Boy kwa sababu wamekuwa na muendelezo mzuri wakuachia nyimbo kali.
Kwenye mahojiano hivi karibuni Nadia amesema wana nyimbo nyingi ambazo hazijatoka ambapo amewataka mashabiki wakae mkao wa kula kupokea EP yao ya pamoja ambayo ameitaja kuwa moto wa kuotea mbali.
Katika hatua nyingine ametupasha kuhusu maendeleo ya album yake mpya kwa kusema kwamba album yake hiyo ipo kwenye hatua za mwisho kukamilika na itakuwa ya kitofauti sana kwani itaangazia safari yake ya maisha kabla na baada ya umaarufu.
Hitmaker huyo “Maombi” amesema album hiyo ilipaswa kutoka mapema mwaka huu lakini kutokana na yeye kushikika na majukumu ya malezi aliamua kuachia EP iitwayo Bundle of Joy ambayo ilikuwa mahsusi kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya mtoto.