
Mwanamuziki nyota wa Bongofleva , Nandy, ameonyesha kuwa bado ana upendo na heshima kwa Yammi licha ya kumaliza rasmi mkataba wa kimuziki na nyota huyo wa muziki.
Kupitia Insta Story kwenye ukurasa wake wa Instagram, Nandy ambaye mkurugenzi wa lebo ya The African Princess amempongeza Yammi kwa siku yake ya kuzaliwa, akimtakia kheri na mafanikio katika maisha na muziki, ikiwa ni ishara ya kudumisha mahusiano mema nje ya kazi.
“Happy born day msanii, keep shining @yammitz,” aliandika Nandy.
Ujumbe huo umekuja wakati mashabiki wakifuatilia kwa karibu mahusiano kati ya wawili hao, kufuatia kuondoka kwa Yammi kutoka kwenye lebo hiyo aliyokuwa chini yake kwa muda na kujipatia umaarufu kupitia nyimbo kama “Namchukia” na “Tunayoyaweza”.
Mapokezi ya ujumbe huo yamekuwa chanya, huku mashabiki wakisifia ukomavu wa Nandy kama kiongozi wa sanaa na mfano wa kuigwa katika kudumisha heshima hata baada ya ushirikiano wa kikazi kufikia mwisho.
Hadi sasa, Yammi hajajibu hadharani ujumbe huo, lakini wengi wanatarajia kuwa hatua hiyo ni mwanzo wa ukurasa mpya wa amani na heshima kati ya wasanii hao wawili waliowahi kushirikiana kwa karibu.