
Rapa maarufu Nicki Minaj amefunguka kuhusu changamoto kubwa alizokumbana nazo katika maisha yake ya muziki. Katika mahojiano na Vogue Italia, Minaj amesema kuwa mara kadhaa alifikiria kuacha kabisa kazi kutokana na ukosoaji wa mara kwa mara na shinikizo la umaarufu. Amesema kuwa licha ya mawazo hayo ya kukata tamaa, aliamua kuendelea kusonga mbele.
“Nimesikia ukosoaji mwingi kuhusu mimi na kazi yangu. Nimewaza kuacha muziki mara nyingi, lakini najivunia kusimama imara na kuendelea.”, Minaj alisema
Katika maelezo yake, Minaj amegusia namna alivyolazimika kuchelewesha uamuzi wa kuwa mama ili kutimiza ndoto zake na kusaidia familia. Anasema japokuwa baadhi ya wanawake hawajuti kuchelewa kuanzisha familia, kwake ilikuwa ni hali ngumu iliyoambatana na majuto fulani.
“Kama mwanamke, nilichelewesha kuwa mama, jambo ambalo baadhi ya wanawake katika tasnia yetu wamelikumbana nalo pia,” alisema. “Wengine hawajutii kuchelewa, lakini mimi niliona gharama zake.”
Akiwa sasa mama wa mtoto mwenye umri wa miaka minne, kupitia ndoa yake na Kenneth Petty, Minaj anakiri kuwa alikosa nyakati nyingi muhimu katika maisha kama vile sikukuu, mapumziko na hatua muhimu za kibinafsi, kutokana na kujitolea kikamilifu katika kazi yake ya muziki. Licha ya hayo, anaeleza kuwa anajitahidi kumpa mwanawe maisha yenye utulivu na fursa alizokosa yeye mwenyewe alipokuwa anatafuta mafanikio.
“Nililazimika kukosa sherehe za familia na likizo kwa sababu ya kazi yangu. Gharama kubwa ilikuwa kukosa maisha ya kawaida,” aliongeza.
Kauli hii ya Minaj imepokelewa kwa hisia mseto mtandaoni, huku mashabiki wakimpongeza kwa ujasiri wake na uwazi katika kushiriki changamoto za maisha yake binafsi. Wengine wamelitumia tukio hili kuibua mjadala kuhusu gharama za umaarufu kwa wanawake katika tasnia ya burudani.