
Rapa Offset ameibua mjadala mpya kwenye sakata lake la talaka na Cardi B baada ya kuwasilisha hati mpya mahakamani akitaka kulipwa msaada wa kifedha (spousal support) kutoka kwa mke wake wa zamani. Kulingana na ripoti mpya ya TMZ, Offset hajataja kiasi anachotaka hadharani, lakini imeelezwa wazi kuwa anahitaji malipo hayo kutoka kwa Cardi B.
Hatua hii inaashiria mabadiliko makubwa katika mwelekeo wa talaka hiyo, ambayo ilianza kwa utulivu mnamo Agosti 2024 baada ya Cardi B kuwasilisha ombi la kuachana rasmi na rapa huyo. Lakini sasa, hatua ya Offset kudai msaada wa kifedha inaonyesha kuwa hana mpango wa kuondoka mikono mitupu katika mchakato huo.
Licha ya ombi lake la msaada wa kifedha, Offset bado anataka malezi ya pamoja ya watoto wao watatu. Hili linaonyesha kwamba, pamoja na tofauti zao, bado anataka kuwa sehemu ya maisha ya watoto wao kwa karibu.
Offset bado hajazungumza hadharani kuhusu ombi hilo jipya, lakini Cardi B alionekana kutoa ishara zisizo za moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii, ambapo alichapisha picha kadhaa kwenye Instagram instastory, hatua ambayo mashabiki wengi wameitafsiri kama majibu ya kimya kwa taarifa hiyo.
Wakati mashabiki wakisubiri kauli rasmi kutoka kwa wawili hao, hali ya mvutano kati ya mastaa hawa wawili maarufu inaonekana kuongezeka, huku pesa na watoto vikibaki kuwa kiini cha mvutano huo wa talaka.