Mchungaji maarufu wa Jijini Nairobi, Victor Kanyari, amezidi kugubikwa na majonzi kufuatia kifo cha aliyekuwa mke wake na mwanamuziki wa injili, Betty Bayo.
Katika video zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii, Kanyari ameonekana akishindwa kujizuia kutokana na huzuni kubwa iliyompata baada ya kusikia taarifa za msiba huo huku wasanii na marafiki wa marehemu wakijumuika naye kumpa faraja..
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Kanyari ameeleza maumivu yake kwa maneno yaliyojaa huzuni, akisema kwamba kifo cha Betty kimemuacha na pengo kubwa lisilozibika. Amesema msanii huyo ambaye ni mama ya watoto wake atabaki daima kuwa sehemu ya familia yake licha ya changamoto walizowahi kupitia pamoja kipindi cha ndoa yao.
Mchungaji huyo mwenye utata, ameongeza kuwa ataendelea kubeba kumbukumbu, upendo na roho ya marehemu moyoni mwake, akimtakia pumziko la amani.
Kanyari na Betty Bayo walikuwa wametengana miaka michache iliyopita kutokana na tofauti za kifamilia, lakini waliendelea kuwa marafiki na wazazi wenza waliokuwa na ushirikiano mzuri katika malezi ya watoto wao.
Licha ya Bayo kuolewa tena, wawili hao waliendelea kushirikiana kwa amani katika kuwalea watoto wao, akiwemo binti yao Sky, ambaye Kanyari alimrejelea katika ujumbe wake wa rambirambi.