Msanii chipukizi kutoka Tanzania, Pipi Jojo, amefichua mipango yake ya kuanza ziara ya kimuziki nchini Uganda kwa ajili ya kutangaza EP yake mpya iitwayo “I Want My Mama Proud.”
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Pipi Jojo ameonekana akizungumza kwa simu na baba yake, Chief Godlove, akimuomba magari manne kwa ajili ya kufanikisha media tour hiyo pamoja na kuandaa dance challenge ya wimbo wake “Chakacha”, ambao video yake ina zaidi ya views milioni moja ndani ya muda mfupi.
Katika mazungumzo hayo yaliyovutia mashabiki, Pipi Jojo ameonekana akideka huku baba yake akimhakikishia kumpatia magari manne ya kifahari pamoja na fedha za kutosha kufanikisha ziara hiyo, ingawa alikiri alitamani kumkodishia ndege binafsi (private jet).
Billionea Chief Godlove, amemsifu binti yake kwa juhudi na nidhamu anayozionyesha katika kazi yake ya muziki, akitabiri kuwa huenda akawa msanii wa kwanza kuipatia Tanzania tuzo ya Grammy.
Kwa sasa, Pipi Jojo yupo katika hatua za mwisho kukamilisha ziara yake nchini Kenya, ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kumjenga kimataifa na kumletea mashabiki wapya kutoka mataifa mbalimbali.