Posta Rangers imevunja msururu wa mechi nne bila ushindi, baada ya kuibwaga Bidco United kwa bao moja bila majibu kwenye mchuano wa Ligi Kuu ya Kenya uliochezewa uwanjani Moi Kasarani Annex, jijini Nairobi.
Bao hilo la pekee lilipachikwa wavuni dakika ya 30 na Brian Otieno, na likatosha kuihakikishia Rangers alama zote tatu muhimu.
Bidco United walijaribu kusawazisha bila mafanikio, huku Rangers pia wakishindwa kuongeza bao la pili licha ya kuonekana kutawala sehemu kubwa ya mchezo.
Ushindi huo umeinua Posta Rangers hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, wakiwa na alama 16—pointi tatu tu nyuma ya vinara Gor Mahia. Bidco United kwa upande wao wameshuka hadi nafasi ya tisa baada ya kichapo hicho.
Ligi Kuu itaendelea Ijumaa, ambapo Posta Rangers watakuwa uwanjani dhidi ya Nairobi United, huku Tusker wakitarajiwa kuvaana na Ulinzi Stars.
Baada ya raundi kumi, Gor Mahia wanaendelea kuongoza ligi wakiwa na alama 19, wakifuatwa na Kakamega Homeboyz pamoja na mabingwa watetezi Kenya Police.