Msanii wa Bongo Fleva Rayvanny amepiga show kali mjini Kigoma, kitendo kilichoonekana kuvunja kabisa wimbi la baadhi ya Watanzania waliodai kususia nyimbo na burudani za wasanii wa Bongo Fleva wanaodaiwa kujihusisha na masuala ya kisiasa.
Kupitia mitandao ya kijamii, Rayvanny amewashukuru watu wa Kigoma hasa vijana wa Gen Z kwa upendo mkubwa waliomuonesha, akisema sapoti hiyo ndiyo nguvu yake kubwa katika safari ya muziki. Amesema mapokezi aliyopata Kigoma ni uthibitisho kuwa muziki wake unaendelea kupendwa na kuungwa mkono na Watanzania wengi, bila kujali mijadala inayozuka mitandaoni.
Msanii huyo pia amejivunia mafanikio ya wimbo wake “Mama Tetema”, akibainisha kuwa hadi sasa hakuna msanii aliyefikia rekodi ya wimbo huo, uliotikisa Afrika Mashariki na kuvuka mipaka ya kimataifa. Kwa mujibu wa Rayvanny, mafanikio ya “Mama Tetema” bado yanabaki kuwa historia muhimu katika muziki wa Bongo Fleva.
Rayvanny alikuwa miongoni mwa wasanii waliotoa burudani katika tamasha la Pilau Day, lililoandaliwa na Mbunge Baba Levo, ambapo maelfu ya wananchi walijitokeza kushuhudia burudani hiyo huku wakifurahia muziki na chakula.