Msanii wa muziki wa injili na mtetezi wa haki za binadamu, Reuben Kigame, ameungana na Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya (KHRC) kuwasilisha kesi ya kikatiba kupinga Sheria ya Marekebisho ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Mtandaoni (Computer Misuse and Cybercrimes Amendment Act), 2024.
Kigame na KHRC wanapinga sheria hiyo iliyotiwa saini na Rais William Ruto tarehe 15 Oktoba 2025, wakisema inakinzana na katiba hasa katika masuala yanayohusu faragha, uhuru wa kujieleza, na uhuru wa vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa hoja zao, marekebisho hayo yanaingiza vipengele visivyoeleweka vizuri na vinavyodaiwa kukiuka katiba, ambavyo vinaweza kudhoofisha haki za kidijitali na ulinzi wa faragha kwa Wakenya.
Wameonya kuwa masharti mapya ya sheria hiyo yanaweza kuleta athari ya kuwatisha wananchi wasitumie haki yao ya kujieleza kama ilivyohakikishwa chini ya Kifungu cha 33 cha Katiba, kwa kuwa vinatoa nafasi ya kukamatwa kiholela na kudhibiti maoni yanayokinzana na serikali mtandaoni.
Miongoni mwa vipengele vinavyolalamikiwa ni hitaji la uthibitisho wa lazima wa akaunti za mitandao ya kijamii, ambapo watumiaji watalazimika kuunganisha akaunti zao na hati rasmi za utambulisho zinazotolewa na serikali.
Kigame na KHRC wanasema hatua hiyo ni uvamizi wa faragha na ni sawa na uchunguzi wa kiserikali, hivyo kukiuka Kifungu cha 31 cha Katiba kinacholinda haki ya faragha ya mtu binafsi.