Msanii wa muziki wa injili Ringtone Apoko ameibua mjadala mkubwa baada ya kutoa kauli nzito akiwataka wasanii wakongwe wa injili kuachia nafasi vijana, akidai kuwa wameshindwa kuendeleza na kuupa mwelekeo mpya muziki wa injili, hali iliyosababisha kuporomoka kwa umaarufu wa muziki huo.
Akizungumza kupitia mitandao ya kijamii, Ringtone amesema kuwa tasnia ya muziki wa injili kwa sasa inahitaji damu changa ili kuleta ubunifu, mvuto na sauti mpya zitakazowavutia vijana wa kizazi cha sasa.
Kwa mujibu wa kauli yake, wasanii wakongwe wamekuwa wakitawala tasnia hiyo kwa muda mrefu bila mabadiliko makubwa, jambo ambalo limefanya muziki wa injili kupoteza mwelekeo na ushindani wake kwenye majukwaa ya kidijitali.
Msanii huyo amesisitiza kuwa ukimya wake wa muda mrefu ulikuwa ni ishara ya kutoridhishwa na hali ya muziki wa injili, akidai kuwa kwa sasa muziki huo hauonekani wala kusikika kwa kiwango kinachostahili. Ameongeza kuwa kizazi cha Gen Z kiko tayari kujitokeza, kuanza upya na kutoa nyimbo mpya zitakazoleta uhai na mvuto mpya katika tasnia hiyo.