
Msanii wa muziki wa dancehall kutoka Ghana, Charles Nii Armah Mensah, maarufu kama Shatta Wale, amekanusha madai yanayosambaa kwamba amemtelekeza mama yake mzazi kwa kutompa mahitaji ya msingi.
Akizungumza kupitia podcast ya moja kwa moja, Shatta Wale aliweka wazi kuwa amewahi kumsaidia mama yake kwa njia mbalimbali, ikiwemo kumpatia magari na makazi bora ya kuishi.
“Huyo mama mnayemzungumzia… sidhani kama nyinyi mlishawahi kununulia mama zenu magari. Mimi nimeshanunulia mama yangu magari; nimefanya mambo mengi kwa ajili yake. Lakini katika maisha, kuna kushinda na kuna kushindwa.” alisema katika maelezo yake.
Kauli hiyo inakuja kufuatia tuhuma zilizokuwa zinasambazwa mitandaoni na baadhi ya mashabiki wakidai kuwa msanii huyo mkubwa amemsahau mama yake licha ya mafanikio makubwa aliyoyapata katika muziki.
Shatta Wale ameendelea kusisitiza kuwa anamheshimu na kumjali mama yake, na kwamba watu hawapaswi kuhukumu mambo ambayo hawana uhakika nayo.