
Mwanamuziki na mfanyabiashara Irene Kayemba amekiri wazi kuwa hawezi kuacha kuvuta bangi, akisema ni sehemu ya maisha yake ya kila siku. Kayemba, ambaye pia ni dada wa mwanasiasa mashuhuri Bobi Wine, amesema bangi ni dawa ya asili ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa katika afya yake na mwonekano wake.
Katika mahojiano ya hivi karibuni, Kayemba anadai matumizi hayo yamezuia kuzeeka kwake mapema na kuyafanya mwili wake uendelee kung’aa. Mrembo huyo ameeleza kuwa mbali na kuitumia binafsi, pia huitumia kutibu wanyama wake wanapougua.
“Siwezi kuacha bangi. Ni tiba ya mitishamba. Naweka kwenye chai, na hata naitumia kwa wanyama wangu. Inanisaidia sana, hata muonekano wangu umedumu,” alisema kwa kujiamini.
Hata hivyo, aliwataka vijana kuwa waangalifu na matumizi ya kupindukia ya bangi, akieleza kuwa matumizi ya kuvuta moshi wa bangi kwa kiwango kikubwa ni hatari kwa afya, na akashauri itumike kama dawa kupitia njia mbadala kama kunywa kwenye chai.
Kauli ya Kayemba imezua mjadala kwenye mitandao ya kijamii kuhusu matumizi ya bangi kama tiba ya asili, huku wengi wakisubiri majibu ya mamlaka husika kuhusu kauli hizo kutoka kwa mtu mashuhuri.