Khaligraph Jones Ashinda Tuzo ya Best Lyricist in Africa, Awaangusha Mastaa Wakubwa
Rapa nguli wa Kenya, Khaligraph Jones, ameweka historia kwa kutwaa tuzo ya Best Lyricist in Africa katika tuzo za mwaka huu za 2025 Africa Golden Awards, akiibuka mshindi mbele ya majina makubwa ya muziki barani Afrika. Katika kipengele hicho kilichoandaliwa kwa ushindani mkali, Khaligraph aliwashinda wasanii wakubwa kama Burna Boy (Nigeria), Sarkodie (Ghana), Nasty C (Afrika Kusini), MI Abaga, Olamide, Asake, Emtee, Cassper Nyovest, Stonebwoy, na wengine wengi waliokuwa wakimezewa mate kwa uwezo wao wa kishairi na ubunifu wa maneno. Tuzo hiyo ni ushindi mkubwa si tu kwa Khaligraph mwenyewe bali pia kwa tasnia ya muziki wa hip hop nchini Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla, huku mashabiki wakimpongeza kwa kuonyesha kuwa muziki wa Kenya una nafasi kubwa kwenye jukwaa la kimataifa. Kupitia mitandao ya kijamii, mashabiki wake walimiminika kwa pongezi, wengi wakisema ushindi huo ni wa haki kutokana na ustadi wake wa kubeba ujumbe mzito kwenye mistari na kujituma kwake kwenye sanaa. Khaligraph, anayefahamika pia kama Papa Jones, ameendelea kuwa na ushawishi mkubwa kwenye muziki wa hip hop Afrika, akiwakilisha Kenya kwa nguvu katika majukwaa ya kimataifa. Ushindi huu unakuja kama uthibitisho kuwa kazi yake ya muda mrefu na bidii imelipa. Tuzo za Africa Golden Awards hutambua vipaji bora kutoka bara la Afrika katika nyanja mbalimbali za burudani, na mwaka huu ushindani ulikuwa mkali kuliko wakati wowote.
Read More